IJUE BIBLIA | LISTENING GOD'S VOICE THROUGH GOSPEL SONGS


Breaking News

Friday 20 May 2016

MAANA YA NDOTO 12 KIBIBLIA AMBAZO WATU WENGI HUWA WANAOTA

MAANA YA NDOTO 12 KIBIBLIA AMBAZO WATU WENGI HUWA WANAOTA


Ndoto ni muhimu sana katika ulimwengu wa roho. Tunapokuwa tumelala, miili yetu ndo inalala lakini roho zetu hazilali. Hivyo kunakuwa na mambo mengi ambayo yanakuwa yanatendeka katika ulimwengu wa roho.
Somo la ndoto ni somo pana sana na ni vigumu kuliandika nikagusia kila kipengele. Hivyo lengo la post hii ni kukupa mtaji ili uweze kuelewa maana ya ndoto chache ambazo umekuwa ukiota. Hii itakusaidia hata unapokuwa unaomba.
Kama nilivyosema mwanzo kuna ndoto za kutoka kwa Mungu (Matendo 2:17 "Itakuwa siku za mwisho, asema Mungu, nitawamwagia watu wote Roho yangu, na wana wenu na binti zenu watatabiri; na vijana wenu wataona maono; na wazee wenu wataota ndoto."), ndoto za kutoka kwa shetani (Kumbukumbu 13:1—4 "Kukizuka katikati yako nabii, au mwotaji wa ndoto, akikutolea ishara au ajabu,ikatukia hiyo ishara au hiyo ajabu aliyokuambia akisema, Na tuifuate miungu mingine usiyoijua, tuitumikie hiyo;wewe usiyasikize maneno ya nabii yule, au yule mwotaji wa ndoto, kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, yuawajaribu, apate kujua kwamba mwampenda Bwana, Mungu wenu, kwa mioyo yenu yote na roho zenu zote.Tembeeni kwa kumfuata Bwana, Mungu wenu; mcheni na kushika maagizo yake na kuisikia sauti yake, nanyi mtumikieni na kushikamana naye."), na pia kuna ndoto ambazo ni matokeo ya shughuli nyingi. “Kwa maana ndoto huja kwa sababu ya shughuli nyingi” (Mhubiri 5:3 "Kwa maana ndoto huja kwa sababu ya shughuli nyingi"). Ndoto ambazo zinatokana na shughuli nyingi hazina madhara yoyote kwani ni akili tu ambayo inakuwa inarudia mambo yaliyotokea au yaliyokuwa yanaendelea katika fikra za mtu. Lakini ndoto za kutoka kwa Mungu au kwa shetani siyo ndoto ambazo ni za kupuuza. Lakini je utajuaje ndoto ya kutoka kwa Mungu au kwa shetani??

Ndoto huwa zimegawanyika katika makundi mbalimbali. Makundi makubwa mawili ni:

a. Ndoto ni mlango wa roho za Mungu au za shetani kuingia kwa mtu ambaye anaota. Tunasoma habari za Sulemani kuwa alipokea roho wa hekima ilikuwa kwenye ndoto (1 Wafalme 3:5—15). Mungu alimtokea Yakobo kwenye ndoto na kumwambia mataifa yote watabarikiwa kupitia yeye (Mwanzo 28:10—15). Lakini pia tunasoma jinsi pepo alivyompitia Ayubu akiwa amelala (Ayubu 4). Hapa ndipo utapata lile kundi ambalo mtu anaona ndoto lakini kitu kinakuwa kinaendelea katika ulimwengu wa roho.

b. Ndoto ni moja ya njia rahisi ambayo Mungu anatumia kuwasiliana na wanadamu. Zamani Mungu alikuwa anaongea na watu kupigia manabii lakini siku hizi Mungu anasema nasi kupitia Yesu Kristo (Waebrania 1:1—2). Mwandishi anaposema Mungu kusema nasi kupitia Yesu maana yake anasema nasi kupitia neno. Kumbuka “kusikia huja kwa neno la Kristo” (Warumi 10:17). Kwa sababu watu wengi hawana neno, Mungu anatumia ndoto ambayo tafsiri yake ipo kwenye neno lake. Ndo maana hakuna ndoto ambayo unaweza kuota isiwe na jibu kwenye biblia, haipo. Iwe imetoka kwa Mungu au imetoka kwa shetani.
Njia pekee ya kuelewa ndoto zako zina maana gani, ni kuwa na neno la kutosha ili uweze kusikia sauti ya Mungu. Lakini pia kuwa unamuomba sana Mungu akupe karama ya kutafsiri ndoto. Mfano, unapoota ndoto juu ya mnyama fulani kama nyoka, inabidi uelewe nafasi ya nyoka katika ulimwengu wa roho baada ya Mungu kufanya uumbaji. Ukitoa ng’ombe anakukimbiza, inabidi uelewe ng’ombe ni nini kibiblia. Lakini pia kitendo kinachotokea kwenye ndoto nacho kinaweza kukuambia maana halisi ya ndoto. Mfano, ukiota unakimbizwa na nyoka na umeumwa na nyoka hizo ni maana mbili tofauti.
Zifuatazo ni ndoto ambazo huwa zinatokea kwa watu wengi. Tuangalie maana zake kibiblia.

1. NYOKA: 
Nyoka ni mnyama aliyelaaniwa kuliko wanyama wote (Mwanzo 3:14). Mungu alimwambia nyoka “nitaweka uadui kati yako na mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino” (Mwanzo 3:15). Hivyo kitu kikubwa nyoka anawinda kwako ni kisigino. Itabidi ufahamu nafasi ya miguu katika ulimwengu wa roho. Ili uweze  una kuelewa kwa nini nyoka anawinda miguu. Hivyo nyoka anapokuwa anakukimbiza, lengo lake ni kukuponda kisigino ili apitishe roho fulani ya shetani. Kuna roho mbalimbali ambazo zinaweza kupita kupitia nyoka. Roho Mtakatifu pekee ndiye anayeweza kukuambia ni roho ipi ilikuwa inapitishwa. Lakini ukiota nyoka amekuuma kabisa, maana yake ile sumu imeingia tayari katika mwili wako na uwe na uhakika utapata matatizo.
Lakini pia ukubwa wa nyoka una maana. Mfano unapokimbizwa na nyoka mmoja wa kawaida tunaongea pepo. Lakini unapokimbizwa na nyoka wengi au uko mazingira ya nyoka wengi, tunaongelea jeshi la mapepo (Angalia Waefeso 6:12). Unapoota nyoka mkubwa kama Cobra au Python inasimama badala ya mfumo fulani wa kipepo. Ukiota nyoka mmoja mkubwa mwenye vichwa 7 vita yako ni dhidi ya Lucipher mwenyewe, malaika aliyetupwa. “ikaonekana ishara nyingine mbinguni; na tazama, joka kubwa jekundu, alikuwa na vichwa saba na pembe kumi, na juu ya vichwa vyake vilemba saba” (Ufunuo 12:3). Ukiendelea kusoma utagundua huyu joka anayeongelewa ni shetani.
Hivyo kama unafatiliwa na nyoka usiku, katika maombi yako uwe unatamka pepo maneno kama “pepo nyoka ambaye...” Na kumbuka kila unapo omba au kuombea mtu fulani siku moja na Mungu akakuonesha nyoka ameketi tumboni mwa mtu huyo katika ulimwengu wa roho. Sasa Mungu anapokuonesha, lazima umtoe huyo pepo uliyeoneshwa. Wengi huwa wanasema tu “kwa jina la Yesu pepo toka.” Pepo yupi unamwambia atoke?? kama hujui pepo unayemtoka hata kama una nguvu kiasi gani pepo hatoki atanyamaza tu kisha ataendelea kusumbua..

2. KUTUMBUKIA SHIMONI
Rubeni akwaambia, Msimwage damu; mtupeni katika birika hii iliyopo nyikani, wala msimguse; ilia pate kumwokoa katika mikono yao, akamrudishe kwa baba yake” (Mwanzo 37:22).
 “Basi wakamtwaa Yeremia, wakamtupa katika shimo na Malkiya, mwana wa mfalme, lililo katika uwanda wa walinzi; wakamshusha kwa kamba. Na mle shimoni hamkuwa na maji, ila matope tu; naye Yeremia akazama katika matope hayo” (Yeremia 38:6). 
Na kwa habari zako wewe, kwa sababu ya damu ya agano lako, nimewatoa wafungwa wako katika shimo lile lisilo maji” (Zekaria 9:11).
Nimekupa mistari hiyo makusudi ile ikupe mwangaza ya nini maana ya kuwa shimoni. Shimo inasimama badala ya kifungo ambacho wewe mwenyewe huwezi kujitoa mpaka msaada kutoka nje. Unapoota upo shimoni, inategemea nani alikutupa shimoni. Kama umetumbukia mwenyewe, chimbuko la kifungo chako ni wewe mwenyewe. Kama rafiki zako au ndugu zako wamekutupa shimoni, maana yake wao ndo chanzo cha kifungo chako. Kuna utofauti kuwa katika shimo lisilo na maji na shimo lililo na maji au matope.

3. CHAKULA: 
Tena itakuwa kama mwenye njaa aotapo, kumbe anakua, lakini aamkapo, nafsi yake haina kitu” (Isaya 29:8). Siyo kila ndoto ya kula ni mbaya ila kuota ndoto unakula na watu huwafahamu au na wafu.  Kumbuka hata Yesu alipokuwa katika karamu ya mwisho na wanafunzi wake walikula chakula. Hivyo ukiota unakula, angalia kitu gani kinatokea baada ya kuamka.Angalia pia nini unachokula na nani unakula naye..
Kwa maana chakula hufanya agano kati ya wale wanaokula chakula huleta mapatano ya kindoa kiroho,mnakua ndugu na wale mnao kula nao chakula.
Chakula kina maana kubwa sana katika ulimwengu wa roho. Ndo maana kuna kiwango fulani ukifikia Mungu hawezi kukuruhusu ule chakula sehemu yoyote. Katika ulimwengu wa roho, unapokuwa unakula chakula unakuwa unafanya ushirika pamoja na wale unaokula nao. Wana wa Israel walipotengeneza mungu wa ndama walikula na kunywa Na Musa alipowakuta alivunjavunja yule ndani akawa majivu akakoroga maji yake akawanywesha wana Israeli (Angaalia maandiko). Unadhani kwa nini Mungu anasema “Wala usingie ndani katika nyumba yenye karamu, kuketi pamoja nao, na kula na kunywa” (Yeremia 16:8). Sehemu zingine utaona Mungu anakataza “Usiingie ndani ya nyumba yenye matanga, wala usiende kuwaombolezea, wala kuwalilia (Jer 16:5).

Kumbuka katika kitabu cha Jeremiah hii sura ilikuwa inalenga kundi fulani la watu. Hivyo haina maana usiende kwenye sherehe yoyote na kula. Ndo maana siyo kila ndoto ambayo unakula ni mbaya. Kinachofanya iwe mbaya ni “je unakula nini na akina nani?” au “nani kaandaa chakula?” Kama unaota unakula na watu waliokufa, maana yake huwa unafanya ushirika na wafu katika ulimwengu wa roho. Halafu hujui unachokua unaingiza  tumboni mwako.

Kwenye suala la kula kwa ujumla siyo kila sehemu unatakiwa ule. Kuna watu ambao wana tabia ya kula kila sehemu. Kwenye misiba, kwenye sherehe, kwenye harusi, hata kwenye sherehe ambazo hawajaalikwa wao wanakula tu. Kabla hujala, hakikisha umepata kibali kutoka kwa Roho Mtakatifu juu ya chakula unataka kula. Wengi wanaokula kwenye sherehe wakidhani wanakula chakula cha sherehe lakini hawajui maana yake katika ulimwengu wa roho. Ukiwa na neno, mambo haya yote biblia imeongelea. Mbaya ni wale ambao wanakula au wanalishwa nyama za watu au za nyoka katika ndoto. Hakikisha unaelewa maana yake.
Maana yake hicho ni kitu unafanya katika ulimwengu wa roho. Hakikisha unayajua madhara yake (Angalia maandiko yanasemaje juu ya nyama – Walawi, warumi, Mithali, 1 Timothy, Kumbukumbu na vingine vingi vimeongelea juu ya nyama). 
Utakula, lakini hautashiba; na fedheha yako itakuwa kati yako nawe utahama, lakini hutachukua kitu salama; na hicho utakachochukua nitakitoa kwa upanga” (Mika 6:14). Pia angalia Hagai 1:6; Hosea 4:6. Je huwa unaota sana unakula? Ulichukua uamuzi gani au uliridhika na hizo ndoto?

4. SHULENI: 
Ukisoma kitabu cha Daniel utaona mfalme alitoa amri ili waletwe vijana wenye sifa fulani na kisha wapelekwe shule kwa muda wa miaka mitato. Lengo la kuwapeleka shule ni ili kuwaandaa ili waje kusimama mbele ya mfalme (Daniel 1). Kwa hiyo shule inakuandaa kwa ajili ya ya hatua ijayo ya maisha. Mfano, ukiwa chuo, unakuwa unaandaliwa ili uweze kuwa mfanyakazi fulani. Kuna uhusiano mkubwa sana kati ya elimu na ndoto za shule.
Wengi huwa wanaota wapo madarasani au mazingira ya shule ambazo zipo kwenye level ambazo walishavuka. Mfano, wewe una familia yako unaota upo shule ya msingi. Unapoota upo darasani au mazingira ya shule ambayo ulishavuka, maana yake katika maisha yako, kuna level ambayo bado hujaivuka kimaisha. Mahali ulipo sipo unapotakiwa uwepo. Ndo maana kama huwa unaota ndoto za namna hii, lazima kuna mambo fulani katika maisha yako ambayo hayaendi vizuri. Hivyo unapokuwa unaomba, unatakiwa uwe unalenga sehemu maalumu katika maombi na kujitoa huko katika ulimwengu wa roho. Kumbuka chanzo cha mafanikio yako ni ulimwengu wa roho, hivyo kama unaota upo level ya chini, maana yake huko ndipo ulipo.

5. KURUDISHWA NYUMBANI: 
Pia watu wengi huwa wanaota wanarudi nyumbani kwao. Mfano mtu anaota yupo kijiji ambacho baba au mama anatokea. Unapoota ndoto upo kwenye kijiji, hiyo inakuambia kuwa vita yako katika ulimwengu wa roho chimbuko lake ni huko. Mfano ukiota umeenda kijiji cha babu mzaa mama, maana yake chanzo cha kukwama kwako katika ulimwengu wa roho ni kwenye kizazi cha mama yako. Hivyo yamkini kuna maagano ya kizazi cha mama ambayo utakuwa umeunganishwa kihalali au pasipo kihalali. Mungu anajaribu kusema na wewe ili uweze kutoka lakini wengi hawajui cha kufanya kwa sababu hawana neno. Ukiota ndoto ya namna hii, jiombee na kujitoa kwenye ushirika na watu wa nyumbani kwenu. Kama maagano na miiko ya kimila.

6. KUFANYA TENDO LA NDOA AU KUFUNGA NDOA:
 Hizi ni ndoto mbaya. Kuna watu wanaota wapo wanafanya mapenzi na wakiamka sehemu zao za siri zinakuwa kama walikuwa wanafanya tendo hilo. Maana yake hiyo haikuwa tu ndoto ila ni kitu ambacho kilikuwa kinafanyika siyo tu katika ulimwengu wa roho bali kiuhalisia. Moja ya madhara ni kuleta matatizo sana katika ndoa. Tuchukulie katika hali ya kawaida. Mume akiwa na wanawake wengine wengi, hiyo ndoa lazima itakuwa ya shida sana.
Hivyo hata unapokuwa unaota, maana yake unakuwa unashiriki nao hicho kitendo katika ulimwengu wa roho. Mwingine anaota amefunga au amefungishwa ndoa na watu asiowajua. Maana yake katika ulimwengu wa roho, huyu mtu tayari yupo katika ndoa za kipepo. Kama tayari uko katika ndoa na unaota ndoto za namna hii, lazima utakuwa na matatizo mengi sana katika ndoa yako. Kama huwa unaota hizi ndoto, angalia jinsi ndoa yako ilivyo. Lakini kama hujafunga ndoa na unaota unafungishwa ndoa na watu huwajui, maana yake katika ulimwengu wa roho, tayari wewe una ndoa ya kipepo.
Moja ya madhara utayoyapata ni tatizo la kuoa/kuolewa au kuzaa. Haijalishi wewe ni mzuri kiasi gani lazima wanaume watakuwa wanakuja na kukuacha au wengine hawaji kabisa. Sababu ni kwamba unataka ufunge ndoa ya pili: ya Mungu na ya miungu. Lazima kwanza uvunje ndoa ya miungu katika ulimwengu wa roho. Hivyo katika maombi yako, tumia damu ya Yesu kuvunja ndoa, kufuta sahihi zote za kipepo, unguza vyeti vya ndoa za kipepo kwa moto wa mbingu, vua pete na utumie damu ya Yesu kusafisha kidole chako.Na ndio maana Yesu alimwaga damu yake ya ubavumi alipochomwa mkuki ni kwa ajili ya kurudish husiano za kindoa kuanzia katika ulimwengu wa roho.

7. NDOTO ZA KUFA: 
Ndoto za kufa ni moja ya ndoto mbaya kuliko ndoto zote kwani zinakuambia kuwa roho ya mauti inakutafuta wewe au mtu fulani. Kwa wale mnaoifahamu biblia, mnajua kuwa mauti na kuzimu zinafanya kazi pamoja katika ulimwengu wa roho. Hivyo roho ya mauti inapokuwa inakujia, kuzimu inakuwa tayari kukupokea katika ulimwengu wa roho. Ukiwa unaota ndoto hizi, kuna kipindi unakuta mawazo yako yote unawaza kifo.
Kuna watu ambao waliwahi kuota ndoto hizo na hawakuamka tena. Hujawahi kusikia mtu amekufa ghafla? Maana yake roho ya mauti imechukua maisha ya mtu huyo. Lakini kama unaota ndoto za aina hiyo haina maana itatokea kama kwenye ndoto, hapana. Inakuambia tu kuwa hiyo roho ya mauti inakuzunguka. Sababu inayokufanya uweze kuamka salama ni kwa sababu ya ulinzi wa Mungu kwakua Mungu hakuruhusu. Siyo kila msiba ni kusudi la Mungu. Kuna kipindi unakuta kijana wa miaka 20 haumwi wala nini ghafla amekufa katika mazingira ambayo hayaeleweki. Halafu watu tunasema “tulimpenda, lakini Mungu alimpenda zaidi.” Siyo kweli.
Kuna vifo vingine chanzo chake ni shetani. Kumbuka habari za Ayubu pale Mungu alipomtoa kwa shetani akamjaribu. “BWANA akwambia Shetani, Tazama, yeye yumo mkononi mwako; lakini tunza uhai wake” (Ayubu 2:6). Kwa hiyo Shetani ana uwezo wa kuondoa uhai wa mtu. Na moja ya njia anaweza kutumia ni kupitia ndoa. Hivyo kama unaota ndoto za aina hii, hakikisha unajitenganisha na roho ya mauti. Maombi yangu kwako ni (2 Timoteo 1:7 "Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi.").

8. KUKIMBIZWA NA NGO’MBE: 
Ukitaka kuelewa ndoto zinazohusu ng’ombe, soma habari za ndoto ya Farao katika kitabu cha Mwanzo 41 au muelewe ng’ombe katika maisha yetu ya kawaida. Unapoota ndoto ya ng’ombe, maumbile ya ng’ombe yana maana tofauti. Tuchukulie katika uhalisia. Ng’ombe akikukimbiza akakumata atakufanya nini? Atakujeruhi kwa kukupiga kwa pembe au kichwa. Kumbuka biblia inapoongelea kujeruhiwa inaongelewa moyo au nafsi kujeruhiwa baada ya kubeba mambo fulani ambayo yanaumiza (Fatilia somo la Mwakasege juu ya moyo uliojeruhiwa angalia link niliyoiweka kwenye page pembeni itakupeleka moja kwa moja).
Hivyo ukijeruhiwa na ng’ombe kwenye ndoto, jeraha linaloongelewa ni la nafsi. Lakini pia unaweza kuota ndoto ya ng’ombe na ikawa na maana nyingine. Nakumbuka niliwahi kuota ndoto kuwa natakiwa nikate majani kwa ajili ya ng’ombe niwalishe. Kulikuwa na majani mengi sana halafu nikaona joka mkubwa sana mweusi akiingia kwenye yale majani ambayo natakiwa niende kukata kwa ajili ya kulisha ng’ombe. Katika ndoto hii, majani ni neno chakula au neno la Mungu, ng’ombe ni watu na joka ni shetani. Joka alipoenda kwenye majani maana yake ni vita ambayo shetani ataileta wakati mimi naifanya kazi hii. Lakini pia ukiota kwa mfano ng’ombe amezaa, au unakamua maziwa na mambo mengine, hizi ndoto zina maana tofauti kabisa. Hivyo ndoto za ng’ombe zinategemea na jinsi ndoto ilivyokuja kwani zipo ambazo zina maana baraka na zingine siyo za baraka.

9. KUKIMBIZWA NA WATU:
 “Tazama, umenifukuza leo katika uso wa ardhi, nitasitirika mbali na uso wako, nami nitakuwa mtoro na mtu asiye na makao duniani; hata ikiwa itakuwa kila anionaye ataniua” (Mwanzo 4:14). “Nanyi mtawafukuza adui zenu, nao wataanguka mbele zenu kwa upanga” (Walawi 26:7). “Matisho yatamtia hofu pande zote, na kumfukuza karibu na visigino vyake” (Ayubu 18:11).
Saul alipotaka kumuua Daudi, tunasoma kuwa “Hivyo Daudi akakimbia, akajiponya, akamwende Samweli huko Rama, akamwambia hayo yote Saul aliyomtenda” (1 Samuel 19:18). Nimekupitisha kwenye hiyo mistari ili uone kuwa unapokuwa unakimbizwa na watu hii inakuambia juu ya maadui zako wa kimwili ambao unawaona katika ulimwengu wa roho. Mara nyingi watakukimbiza lakini hawatakukamata. Wanaweza kuwa watu unaowafahamu wakati mwingine usiowafaham. Utaona katika maandiko, mtu aliyekuwa anakimbizwa, alikimbia ili kuikoa nafsi yake kutoka kwa adui wa mwili, siyo adui wa roho kama mapepo.

10. KUOGELEA: 
Siku moja niliota rafiki yangu mmoja yupo anaogelea kwenye mto na anaenda opposite na mkondo wa maji. Nilipoota hiyo ndoto, nilielewa kabisa kuwa ana mambo mengi sana yanamsonga na ana-struggle. Kesho yake mimi nilichomwambia ni kwamba “naona una mambo mengi sana right now.” Ndipo akaanza kuniambia mlolongo wa mambo yote anatakiwa kufanya. Lakini kwa sababu Mungu alishanionesha, nilichofanya ni kumuombea ili Mungu ampe nguvu aweze kufanya mambo yote ili moyo wake usilemewe. Watu hatukuumbiwa kuishi majini hivyo ukiota upo majini maana yake kuna mambo fulani katika maisha ambayo unapitia na una-struggle.
Lakini pia inategemea kama unaogelea kwenye swimming pool, baharini, au mto. Lakini pia kuna utofauti kati ya kuogelea kwa kutaka na kuogelea kwa kutotaka. Unapojipeleka mwenyewe kuogelea, hii ni struggle ambayo chanzo ni wewe mwenyewe. Lakini ukijikuta tu unaogelea hapa ni struggle ile ambayo haiji within you. mapambano ya aina yoyote ile yapo ndani ya uwezo wako. Lakini kumbuka kuwa Mungu yupo pamoja nawe katika magumu yoyote. “Upitapo katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe; na katika mito haitakugharikisha; uendapo katika moto, hutatekea; wala mwali wa moto hautakuunguza” (Isaya 43:2). Wakati mwingine unakuwa tu unavuka mto, au bahari, ai dimbwi la maji. Maana yake kuna changamoto ambazo upo unazipitia lakini zinatofautiana. Ukiwa unaogelea na unataka kuzama, hapo maana ni tofauti.

11. PESA: 
Tuchukulie katika hali ya kawaida. Je ukiwa unatembea ukaona hera njia, tuseme 10,000 Tshs utaichukua au utaicha? Jibu ni INATEGEMEA. Kabla hujaichukua lazima uhakikishe Roho Mtakatifu amekuruhusu uichukue otherwise utaicha (wengine utachukua tu). Unaweza kuchukua pesa kumbe ni sadaka ilitolewa kwenye kafara au ni sadaka imewekwa kwa ajili ya mapepo. Sasa imagine hiyo hera wewe unaichukua halafu unaenda kuitumia. Kuna watu wengine wanachukua hera popote pale wanapoona. Hakikisha unajua unachokifanya kwani maandiko yako wazi.
Hivyo hata kwenye suala la ndoto za pesa ni hivyo hivyo. Siyo kwamba kila ndoto ya pesa ni mbaya ila inategemea. Watu wengine wanaenda kwa waganga wakienyeji halafu wanatoa sadaka. Halafu mganga let’s say anachimba then anazika zile pesa kama ishara ya kuzitoa kwa miungu. Katika ulimwengu wa roho, zile pesa zinakuwepo kule. Sasa wewe kwenye ndoto unaota unachimba hera then unazichukua halafu zinakuwa haziishi. Check baada ya kuamka nafsi yako itakuwaje kwani hiyo itakupa jibu tosha.

12. NDOTO ZINAZOJIRUDIA: 
Hizi ni ndoto ambazo mtu unakuwa unakumbusha kitu fulani kinachoendelea au kitachotokea katika maisha yako. Kuna ujumbe ambao Mungu anaweza kuwa anakuambia kwa kurudia. Wengi huwa hawajali hata kama Mungu akiwaambia zaidi ya mara moja. “Kwa kuwa Mungu hunena mara moja, Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu hajali. Katika ndoto, katika maono ya usiku, Usingizi mzito uwajiliapo watu, Katika usingizi kitandani(Ayubu 33:14-15). Ndoto za kujirudia usizipuuzie kwani kuna ujumbe ambao unapewa.
Hakikisha una tabia ya kuandika ndoto kama inawezekana kwani maono yanapokuja, lazima yatatokea. “BWANA akanijibu, akasema, iandike njozi ukaifanye iwe wazi sana katika vibao, ili aisomaye apate kuisoma kama maji. Maana njozi hii bado ni kwa wakati uliamriwa, inafanya haraka ili kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokuwa, ongojee; kwa kuwa haina budi kuja, haitakawia” (Habakkuk 2:2-3).
 Kumbuka kila unakuwa katika ndoto na wewe unauwezo wa kuzuia chochote kibaya kisitokee iwe kwenye ndoto au kihalisia..Acha kauli za ni ndoto tu.. kumbuka somo la WEWE NI NANI? Wewe ni roho na vita ulivyonavyo ni vya kiroho,vivyo hivyo huwezi kufanikiwa katika mwili ikiwa utashindwa katika ndoto pambana mpaka uhakikishe umeshinda ndipo uamuke usikimbilie kuamuka hata kama ndoto inatisha kiasi gani...unaweza kubadili chochote na unaweza kusafiri kwenda popote katika ni kiasi cha kuwaza nawe utakuwa huko kwa kuwa roho haina mipaka na mipaka yake ni mwili..pia kuwa makini sana kwani kila  unachokiona kwenye ulimwengu wako wa mwili ni matokeo ya kilichotokea kwenye ulimwengu wa roho na ndoto ni mlango mmojawapo wa kuingilia ulimwengu wa roho
                          Mungu Aliye mbinguni Akubariki

7 comments:

Victoria Mushi said...

Mungu akuzidishie maarifa

Unknown said...

amen amen barikiwa mtu wa Mungu

Unknown said...

Mgu nakupe marifa zaidi umenisaidia Sana kwa doto ya kiyumbani nimeriota Mara kathaa,

Emmy said...

Amen mtumishi may God bless you

Hadithi za santos said...

barikiwa

Neema dabana said...

Nimejifunza kitu kikubwa.barikiwa sana mtumishi

Unknown said...

God bless you