IJUE BIBLIA | KNOW THE BIBLE
KARAMA ZA ROHO MTAKATIFU~03
Karibu tuendelee;
Bwana Yesu asifiwe…
03.AINA ZA KARAMA ZA ROHO MTAKATIFU.
Karama hizi ni miongoni mwa karama ambazo biblia imeziorodhesha katika 1 Wakorintho 12:8-10. Ili kuelewa vizuri na kupata mpangilio mzuri,basi nimekupangia karama hizi katika makundi makuu manne;
A.Karama za kusema.
(i) Lugha.
(ii) Kutafsiri lugha.
(iii)Unabii.
B.Karama za Ufunuo.
(i) Neno la hekima.
(ii)Neno la maarifa.
(iii)Kupambanua Roho
C.Karama za uwezo.
(i) Karama ya imani.
(ii)Karama za uponyaji.
(iii)Matendo ya miujiza.
Roho mtakatifu ametoa ufunuo mbali mbali kwa kufaidiana kama apendavyo Yeye 1 Wakorintho 12:8.
A.KARAMA ZA KUSEMA.
(i)Karama za lugha
~Karama za lugha nazo zimegawanywa katika sehemu kuu mbili;
▪Lugha katika kulijenga kanisa, kuhutubu.
Udhihirisho wa Roho wa namna hii ujulikana pia “lugha ya ibada” Hiki ni kipindi cha kuwajenga waamini,kuwatia moyo,kuwatia nguvu kwa maneno yenye kueleweka vizuri (1 Wakorintho 14:3). Sifa mojawapo ya karama hii ni kwamba,ili ifanye kazi inategemea hadhara ya watu walioandaliwa kupokea ujumbe. Kuhutubu,kunamfanya yeye aliye mjinga kupata nafasi ya kuelimika kwa neno la Mungu.
▪ Lugha katika kunena(kunena kwa lugha mpya)
Uhidhihirisho huu ni wa aina ya pili,ni udhihirisho wa Roho mtakatifu katika kunena kwa lugha.Kunena kwa lugha ni kutamka maneno katika Roho yasiyopangwa kutamkika,na yasiyoeleweka maskioni mwa watu hata shetani haelewi kabisaa!isipokuwa roho ya mtu hunena mambo ya siri na Roho wa Mungu~ Matendo 2:4.
Kumbuka;kupo kunena kwa lugha mpya baada ya Roho mtakatifu kushuka (Matendo 19:6,Matendo 2:4) Lakini pia kupo kunena kwa lugha kwa namna ya karama rasmi. Kile ninachozungumzia hapa ni unenaji wa lugha katika karama.
Mtu mwenye karama hii,muda wote aweza kunena kama apendavyo Roho mtakatifu. Haitaji kuanza kutafuta uwepo kwamba aabudu kwa kipindi kirefu ndipo anene,bali anaweza akaabudu kidogo tu kisha akanena,au akawa akinena katika maombi.
(ii) Kutafsiri lugha.
Karama hii inategemea malighafi ya udhihirisho wa Roho mtakatifu wa kunena kwa lugha. Maana ili utafsiri,unahitaji lugha iliyonenwa lakini haikueleweka,au haieleweki katika hadhara husika,ndiposa hitaji la kufasiri hujitokeza. Karama hii inawezeshwa na Roho mwenyewe,kwa sababu hakuna awezaye kufasiri lugha kwa kutumia akili zake mwenyewe pasipo kuongozwa na Roho mtakatifu. Wala hakuna ujanja ujanja unaohitajika katika kufasiri lugha pale lugha mpya itolewayo,ni kwa msaada wa Roho mtakatifu tu.
~Je karama hizi mbili yaani,karama ya kunena katika roho,na kufasiri zinatumikaje?
JIBU;Yapo mazingira mawili ambapo yakupasa kuyajua kwamba ni kipindi gani haswa cha kufasiri lugha na kipindi gani haswa si cha kufasiri lugha pindi mmoja anenapo(na huu ni ufunuo)
Hivyo basi ili tuweze kuyajua haya yote hatuna budi kujua aina za unenaji wa lugha,zipo mbili nazo ni;
(a)Mtu akizungumza na MUNGU wake kwa njia ya lugha.
(b)MUNGU akizungumza na watu wake kwa njia ya lugha.
Tazama,Mtu akizungumza na MUNGU wake kwa njia ya lugha,haitaji mtafsiri maana mtu huyu hunena mambo ya siri katika roho yake,wala hasemi na watu~ 1 Wakorintho 14:2. Lakini,Mungu anaweza kuzungumza na watu wake kwa njia ya lugha akimtumia mtumishi wake,hapa ndipo pana hitaji mwenye karama ya kutafsiri lugha aingie kazini kwa msaada wa Roho mtakatifu ili kuwezesha ujumbe wa Mungu ueleweke kwa watu wote ~ 1 Wakorintho 14:13
(iii)Unabii.
1 Wakorintho 12:10
Hapo zamani mtu mwenye karama hii alikuwa akijulikana kuwa ni “ mwonaji” Imeandikwa“ (Hapo zamani katika Israeli, mtu alipokwenda kuuliza neno kwa Mungu, husema hivi, Haya! Twende kwa mwonaji; maana mtu aitwaye sasa Nabii hapo zamani aliitwa Mwonaji.) “1 samweli 9:
Hivyo basi,karama hii inampa mtu kuona mambo yajayo katika ulimwengu wa roho kwa kadri Roho mtakatifu anavyojifunua kwake. Karama hii ni zawadi nzuri ya kupata taharifa za matukio yajayo,ili uweze kuyashughulikia sasa. Hata kanisa,haliwezi kwenda bila nabii,yeye aonaye mambo ya sirini. Ikumbukwe ya kwamba unabii hautolewi kwa sababu ya mapenzi ya mtu fulani bali kwa sababu ya mapenzi ya Roho mtakatifu;
“ Mkijua neno hili kwanza, ya kwamba hakuna unabii katika maandiko upatao kufasiriwa kama apendavyo mtu fulani tu. Maana unabii haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu.” 2 Petro 1:20-21
ITAENDELEA…
No comments:
Post a Comment