IJUE BIBLIA | LISTENING GOD'S VOICE THROUGH GOSPEL SONGS


Breaking News

Wednesday, 14 September 2016

MAMBO YA KUFANYA/KUZINGATIA KATIKA KIPINDI CHA UCHUMBA

MAMBO YA KUFANYA/KUZINGATIA KATIKA KIPINDI CHA UCHUMBA


Mpenzi msomaji tunakusalimu kwa jina la Yesu!
Baada ya kuwa tumepata maombi ya vijana wengi kutaka kujifunza habari za Uchumba, mke wangu pamoja nami tumeona ni vema tukaandaa somo hili ambalo tunaamini litafanyika msaada kwa vijana wengi ambao wapo kwenye uchumba au wanajiaandaa kuingia katika eneo hili. Hata hivyo somo hili ni pana sana, kwa sasa tumeandika vitu vichache vya msingi, tunaamini kwamba huko mbele tutaandika kitabu chake rasmi.
Katika kitabu cha Muhubiri 3:1 Biblia inasema “Kwa kila jambo kuna majira yake, na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu”. Hivyo mwanadamu katika maisha yake hapa chini ya jua  kuna vipindi mbalimbali anavyovipitia hii ni pamoja na kipindi cha uchumba kwa sehemu kubwa ya watu.
Katika kipindi hiki yapo mambo mengi ambayo wachumba hufanya, mengine ni mazuri na mengine hayafai kabisa. Na hii yote inatokana hasa na mitazamo au tafsiri ya uchumba kwa watu husika. Fahamu kwamba tafsiri unayokuwa nayo juu ya mchumba wako ndiyo inayokuongoza kujenga mahusiano ya aina fulani pamoja naye.
Lengo la somo hili ni;
Kuongeza ufahamu wa wachumba kuhusu kipindi hiki na Kuwapa vijana maarifa ya kuwasaidia kuishi kwa nidhamu ya Ki-Mungu katika uchumba wao. Pia ni kuwafikirisha vijana wanaotarajia kupita katika kipindi hiki mambo ya kuzingatia. Si wachumba wengi wanajua, Mungu anawataka wafanye nini katika uchumba wao au kwa lugha nyingine si wachumba wote wanaojua kwa nini kipindi cha uchumba kipo. Naam katika somo hili tumeandika mambo hayo kinaga ubaga.
Kwa kuwa suala la uchumba ni pana na lina mitazamo mingi, yafuatayo ni mambo tuliyozingatia katika uandishi wa somo hili;
  • Kuna makundi mbalimbali ambayo yana taratibu zao kuhusu mchakato wa mtu kumpata mke au mume kikiwepo kipindi cha uchumba. Makundi hayo ni pamoja na makanisa, makabila, familia nk.
  • Wachumba wanaweza kutofautiana kwa kiwango cha elimu, uchumi, ufahamu juu ya mambo mbalimbali, kikabila, umri na hata kwa rangi pia.
  • Kuna baadhi ya wachumba hadi kufikia muda wanakubaliana kwamba watakuja kuishi pamoja walishafahamiana tangu zamani na wengine hawakufahamiana.
  • Wachumba wanaweza wakatoka katika madhehebu/makanisa tofauti na hili ni kwa kuzingatia madhehebu/makanisa mengi yaliyopo.
Lengo letu ni kuandika juu ya mwongozo wa Neno la Mungu katika kipindi cha uchumba. kwa lugha nyingine, je Mungu anataka wachumba wafanye nini katika kipindi chao cha uchumba?. Kumbuka uchumba ni kipindi/wakati. Basi kama ni wakati jua kabisa kuna baadhi ya mambo ambayo ni lazima yafanyike, kwani Biblia inasema katika Mhubiri 8:5b “ Na moyo wa mwenye hekima hujua wakati na hukumu”, neno hukumu linamaanisha maamuzi, mambo ya kufanya.
Yafuatayo ni mambo ya msingi kufanya katika kipindi cha uchumba;
Jambo la kwanza –  Mruhusu Roho Mtakatifu afanyike Bwana wa uchumba wenu
2Wakorinto 3:17 ‘Basi Bwana’ ndiye Roho; na alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru’.
Kumbuka Roho Mtakatifu ni msaidizi. Hivyo basi ni vema kumtumia vema hasa katika nyanja hii ya mahusiano katika kipindi hiki cha uchumba. Ni Roho Mtakatifu pekee mwenye uwezo wa kukujulisha mambo na siri nyingi kuhusu mchumba wako hata kama yeye hataki kukueleza. Ukimruhusu Roho Mtakatifu afanyike Bwana, yeye atakuongoza katIka kufanya maombi yanayolenga maeneo ya msingi juu ya huyo mwenzako. Kila mtu ameumbwa pamoja na mapungufu fulani au kwa lugha nyingine mapungufu/ udhaifu (weakness) ni sehemu ya maisha ya mwanadamu. Roho Mtakatifu anapokuwa Bwana wa mahusiano yako yeye atakusaidia kuona madhaifu au mapungufu ya mwenzako kama kitu cha wewe kujivunia(Strength) kwa maana ya kuona udhaifu wa mwenzako kama kitu chema na si kibaya.
Kumbuka Paulo katika 2Wakorinto 12:9-10. —‘Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ….kwa hiyo napendezwa na udhaifu——- maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu. Hivyo Roho Mtakatifu atabadilisha tafsiri ndani yako za vyote unavyoona kwa mwenzako huenda juu ya umbile lake, umri wake, macho yake, kabila lake viwe vitu vya wewe kujivunia. Zaidi Roho Mtakatifu pia atakuongoza katika maombi yatakayosidia kuuondoa ule udhaifu ambao umekuja si katika mapenzi ya Mungu, yaani wa kishetani.
Jambo la pilini wakati wa kuweka msingi imara wa uchumba wenu na kufahamiana zaidi.
Hili jambo ni la muhimu  kuzingatia. Ni vema wachumba wakatafsiri na kuelewa vizuri maana ya uchumba. Wachumba wanapaswa kuwa na mipaka fulani katika uchumba wao na  kuwa makini kwa kujilinda na mazingira ya kila namna ambayo yanaweza yakapelekea wao kuanguka dhambini. Ni vema mkajua kwamba ninyi ni wachumba na si wanandoa. Na kama ni wachumba basi uchumba una mipaka yake na hamruhusiwi kufanya mambo ya wanandoa. Mipaka hii iwe kwa habari ya kutembeleana,kupeana zawadi, mawasiliano (ingawa mnapaswa kuwa makini na lugha mnazotumia pia) nk.  Lengo la kutafsiri misingi ya mahusiano yenu ni kujiwekea mipaka na mazingira yatakayowasaidia kuishi maisha ya nidhamu, ushuhuda na kumletea Mungu utukufu.
Sambamba na hili sehemu kubwa ya wachumba huwa wanakuwa hawafamiani vizuri. Japo wapo baadhi ambao walianza tangu shule za msingi/sekondari/chuo na sasa wamechumbiana hivyo kwa sehemu wanafahamiana vema. Kwa wale wasiofahamiana vema huu  ni wakati wa kumjua mwenzako vizuri kwa maana ya kabila lake, familia yake, umri wake, interest zake, matatizo aliyo nayo yeye binafsi au ya kifamilia, mitazamo yake juu ya mambo mbalimbali kama uchumba, ndoa, maisha, wokovu, neno la Mungu nk. Huu ni wakati wa kumjua mwenzako kwa njia ya maswali mbalimbali ya msingi yanayohusu vitu nilivyovitaja hapo juu. Lengo hapa ni kujua mapungufu/madhaifu(weakness) na mazuri(Strength) za mwenzako ili mjue namna ya kukabilana na mapungufu na namna ya kuendeleza yaliyo mazuri.
Ni vema pia kuulizana historia zenu za maisha ya nyuma. Kabla ya kuokoka umepitia katika mifumo gani ya maisha ambayo imechangia kukufanya uwe ulivyo. Kabla ya kumpata uliye mpata ulikuwa umefuatwa na wangapi na uliwakubalia au la, na kama uliwakubali kwa nini mliachana, na sasa wako wapi, je bado wanakufuatilia. Hii itawasaidia sana kujipanga vizuri kimaombi na katika mahusiano yenu na zaidi itawasaidia kuweza kuchukuliana na kuhifadhiana katika madhaifu ya kila mmoja.
Mungu anapowaunganisha anakuwa na kusudi maalum. Hivyo jua kwamba huyo mwenzi uliyepewa umepewa kwa ajili ya kusudi fulani la Mungu. Ni wachumba wachache sana ambao pindi wanapokutana kila mmoja anakuwa anajua walau kwa sehemu kwa nini aliumbwa. Sasa ni vema mkae chini mfikiri, nini Mungu anataka kukifanya duniani kupitia ninyi? Na zaidi angalieni kazi zenu au yale mnayoyasomea, Je mtawezaje kuliimarisha agano la Bwana kwa pamoja kama mke na mume?.
Hapa maana yetu mnatakiwa kujibu maswali yafuatayo? Je ni kwa nini mlizaliwa? Je kwa nini Mungu amekuunganisha na huyo uliye naye sasa? Na je kupitia elimu, bisahara zenu au kazi mlizonazo mtawezaje kuimarisha agano la Bwana?, Kwa kuzingatia vipawa na uwezo Mungu aliowapa, je ni wapi Mungu anataka kuwapeleka na kuwafikisha? Kama ndani yenu mna huduma fulani, je ni watu gani ambao Mungu atataka mshirikiane nao katika huduma hiyo?, je ipi ni nafasi yenu katika mwili wa Kristo na taifa kwa ujumla? Ni vema zaidi mwanaume akajua wito/ kusudi aliloitiwa ili pia amshirikishe na mwenzake.
Kufanikiwa kwa hili kunahitaji uwepo muda wa kutosha wa wachumba kukutana ili kupanga na kuweka mambo yao mbalimbali, na kama ni watu walioko mbali basi suala la mawasiliano kwa njia mbalimbali kama simu, barua pepe, na barua na hata zawadi ni la muhimu.
Jambo la tatu– ni wakati wa kulinda wazo la Mungu hadi litimie.
Siku zote uamuzi wowote unaoufanya una gharama. Naam uchumba pia una gharama nyingi Sana za kuzikabili kuliko unavyofikiri. Gharama hizo ni pamoja na muda, pesa, mawasiliano, maombi, uhuru nk. Kumpata mchumba au mwenzi ambaye ni wa kusudi la Mungu, usidhanie ndio umemaliza. Kama huo uchumba wenu ni wa mapenzi ya Mungu muwe na hakika mtakutana na vita kubwa sana katika kipindi hicho cha uchumba na lengo ni kuwatenganisha. Ni lazima mjifunze siku zote kuombeana kwa kumaanisha maana Shetani naye yupo kazini ili kuvuruga hayo mahusiano.
Kumbuka huyo mwenzi ni agano toka kwa Bwana hivyo unawajibika kumlinda, kumlinda ni pamoja na kuhakikisha wewe hausabibishi au haufanyiki chanzo cha ninyi wawili kuanguka dhambini, au ukamwacha na kumsababishia majeraha ya nafsini na hivyo kuharibu mahusiano yake na Mungu. Wapo watu waliofikia kuharibu mahusiano yao na Mungu kisa mchumba, saa ya ibada imefika mchumba anasema twende zetu out bwana, unataka kufanya maombi ya kufunga mchumba anasema kesho nitakutoa out, inagharimu sana muda wa kuwaza pia kwa ajili yake na familia yake au mahitaji mbalimbali aliyo nayo.
Zaidi pia uchumba unaweza kukunyima uhuru hata wa kuwa na maongezi na rafiki zako, maana kuna baadhi ya watu huwa hawataki kuona mchumba wake anaongea au kucheka na watu wengine, na pia kuna wengine ni wachumba lakini wamewekeana taratibu ngumu utafikiri wanandoa kabisa na ukweli zinawatesa ila kwa sababu hataki kumpoteza huyo mchumba wake inabidi avumilie.  Jambo tunalosisitiza hapa ni kwamba, uchumba una gharama nyingi angalia mahusiano yako na Mungu yasiharibikie hapa.
Jambo la nne– ni wakati wa kupanga malengo na mikakati yenu ya baadae.
Mithali 29:18a “Pasipo maono, watu huacha kujizuia’
Hili si jambo ambalo vijana wengi hulipa kipaumbele linavyostahili. Katika hili ni vema wachumba wafikirie mapema ni aina gani ya maisha ambayo wangependa kuwa nayo, na pia je ni aina gani ya ndoa wanataka kufunga, tatu je ni wapi wangependa kuja kuishi kwa maishayaoyote. Haya yatawasaidia wahusika kujipanga ndani na nje kukabiliana na yaliyo mbeleyao.Kamawanataka kufunga harusi kanisani basi maana yake wanahitaji kuwa na maandalizi mazuri kifedha, waweke katika muda kila wanalotaka kuelekea katika harusiyaoili iwasaidie kujiaadaa mapema. Malengo yoyote yale ambayo mtaweka basi hakikisheni yanatekelezeka, yanafikika, yanapimika na mnayapangia muda wa utekelezaji.
Mambo zaidi ya kuzingatia katika malengo yenu;
Katika hili ni vizuri wachumba waangalie nafasi yao kifedha imekaaje, na changamoto zinazowakabili wote kwa pamoja. Je hali yao kifedha inawaruhusu kuzikabili gharama za maandalizi ya ndoa kwa ujumla. Je hali ya kimaisha ya kijana wa kiume inamruhusu wakati wowote baada ya kuchumbia aweze kufunga harusi kama anataka. Je nafasi zao kielimu zikoje, je kama zinatofautiana ni kwa kiwango gani? Na je tofauti zao kiuchumi na kitaaluma zinaweza kuwa kikwazo kwao kuoana, au kwa wazazi wao nk. Na je baada ya kuwa wamegundua na kupima uwezo wao katika hayo mambo mawili, je wanaweza wakasaidianaje ili wafike mahali pazuri wote wawili.
Vijana wengi wa kiume huwa wanakosea sana hapa, wengi huwa wanasema sitaki kuchumbia/kuoa mpaka niwe nimesha jikamilisha kiuchumi, niwe angalau na maisha mazuri. Sisi hatushauri sana dhana hii, ukweli ni muhimu kwa kijana wa kiume akjikamilisha kwa yale mambo ya msingi. Lakini fahamu kwamba kuna wakati mwingine kuendelea kwako kiuchumi, au kuvuka kwako kimaisha ni rahisi zaidi pale unapokuwa na mchumba au ndoa yako. Tunasisitiza tena ni vema wachumba wakae chini na kufikiri ni kwa namna gani wataendelezana kiuchumi na kitaaluma. Angalizo, ni vema uwe na uhakika kweli huyo mtu ni wa mapenzi ya Mungu kwa maana ya kuwa ni wa kwako kweli, maana wapo wachumba ambao wamekuwa wakisaidiana mpaka kulipiana ada, kupeana mitaji, kununuliana nyumba, magari nk, halafu mwishowe mmoja anavunja maagano, maumivu yake ni makubwa sana.
Jambo la tano – ni wakati wa matengenezo na kuzijenga nafsi zenu
Wachumba wengi huwa wanafichana mambo mengi sana wanapokuwa wachumba na matokeo yake hawayashughulikii mapema na hivyo yanakuja kuwaletea shida kwenye ndoa. Huenda kabla hujakubaliwa wewe tayari mwenzako alikuwa amesha wakubali vijana au mabinti wengine kwamba ataolewa nao au kuwaoa. Pia  kama ni msichana huenda ameshawahi kubakwa, au kutokana na masumbufu ya kupata mtu sahihi na wakati mwingine kuachika mara kwa mara imefika mahali huyo msichana akasema sitaki kuja tena kuolewa. Zaidi  huenda  mmoja wenu huko nyuma ameshawahi kufanya uasherati au zinaa kabla hamjachumbiana. Au kuna mwingine amekuwa akisumbuliwa na tatizo la harufu, kufanya tendo la ndoa na mapepo nk.
Haya yote na mengine mengi yanayofanana na haya yana athari kubwa sana kiroho na kimwili kwenu kama wachumba na wanandoa watarajiwa kama hayatashughulikiwa vema katika kipindi hiki cha uchumba. Licha ya kuwa na athari mambo hayo yamepelekea nafsi za watu au wachumba wengi kujeruhika. Nafsi inapojeruhiwa inaharibu ndani ya mtu mfumo wa kufanya maamuzi, mfumo wa utiifu kwa Mungu wake, mfumo wa kunia na kuhisi pia. Sasa mifumo hii inapoharibika inapelekea watu kufanya maamuzi ambayo yapo nje ya mapenzi ya Mungu kabisa. Nawajua baadhi yao ambao wameacha na wokovu, na, wengine wamekata tamaa ya kuolewa, wapo walioamua kuolewa na mataifa ilimradi ameolewa nk.
Hivyo basi tumieni wakati huu kufanya matengenezo na kujengana nafsi zenu kwa maana ya kuombeana sana, pili kwa kuongeza ufahamu wenu katika neno  la Kristo hasa maandiko yanayolenga uponyaji katika nafsi zenu, tatu kufuta na kufisha mapatano/maagano yote ambayo mmoja wenu aliyafanya huko nyuma na watu wengine na pia kufuta picha za kubakwa na kujenga ufahamu wa mtu aliyeathirika kisaikolojia kutokana na mambo kama hayo kwa njia ya Damu ya Yesu. Hatua hizi zitawasaidia kurejesha mifumo iliyoharibika na kuziruhusu nafsi zenu zifanye kazi kama inavyotakiwa.
Jambo la sita – ni wakati wa kujua taratibu mbalimbali kuelekea kwenye ndoa
Tumeshasema, kila dhehebu au kabila wana taratibu zao kuhusu uchumba hadi ndoa. Hivyo ni vema wachumba, wakafuata taratibu ambazo zimewekwa na makanisa yao hasa zile ambazo zipo katika mapenzi ya Mungu. Lakini pia lazima tukubali kwamba kuna baadhi ya taratibu za makanisa, makabila na hata madhehebu ambazo nyingine zipo tu lakini hazitekelezeki na nyingine hazimpendezi Mungu.
Sasa ni vema wachumba wazijue hizo taratibu na wajue je wanaweza kuzitekeleza au la, na kama hawawezi wafikirie kabisa wanafanyeje. Mfano kuna baadhi ya makanisa ambayo hayaruhusu mtu wa kwao aoe au kuolewa na mtu wa nje ya dhehebu hilo. Sasa hii ina maana kama una mchumba wa aina hiyo jipange kujibu maswali ya wazee wa kanisa na Mchungaji vizuri. Na zaidi kuna baadhi ya makabila na familia hazitaki uoe au kuolewa na watu nje ya kabila lako, au aliyekuzidi umri kama wewe ni kijana wa kiume nk. Hivyo ni vema kuzijua hizo taratibu ili mjue mnajipangaje kukabiliana nazo. Ushauri wetu ni huu kama una uhakika huyo mtu ni wa kutoka kwa Mungu basi simamia la Bwana maana lipi jema, kumpendeza Mungu au wanadamu?. Kumbuka Mungu ndiye mwenye ratiba ya kila mmoja wetu.
Suala la  kukagua/kupima afya zenu kwa pamoja.
Kwa mazingira ya ulimwengu wa sasa suala la ukimwi limechukua sura mpya na kuleta mtafaruku ndani ya kanisa hasa kwa vijana wanochumbia kabla ya kupima afya zao. Siku hizi jambo hili limewafanya wachungaji kuomba sana kwa habari ya vijana ndani ya kanisa. Sasa kama mlikuwa hamjapima afya zenu mpaka mmechumbiana basi chukueni hatua mwende kupima. Ni vema wachumba wakapima mapema afya zao ili jambo hili lisije likawaletea shida baadaye, maana kwa sheria ya nchi yetu wachungaji hawaruhusiwi kufungisha ndoa kama mmoja wa wahusika ameathirika.
Upimaji wa afya zenu ni wa muhimu kwani, ndani ya makanisa kuna rekodi ya vijana wengi tu ambao wameshaathirika na huenda si kwa sababu ya zinaa, maana kwa mujibu wa watu wa afya njia za maambukizi ni nyingi. Kuna wengine wamezaliwa nao, kwa nia ya kuongezewa damu,kutumia vifaa kama nyembe, sindano nk. Hata hivyo swali la msingi inabaki kwamba je, liko tumaini kwa mtu aliyeathirika kuoa au kuolewa?
Tukueleze hivi, hakuna jambo gumu lolote la kumshinda Bwana, hii ni pamoja na ukimwi, kama Mungu alimfufua Lazaro, alitenganisha bahari ya Shamu na watu wakapita, kama Yesu alitembea juu ya maji, basi naomba ujue kwamba Ukimwi hauwezi kuzuia kusudi la Mungu hapa duniani kwa wale awapendao na kwa sababu hiyo tunasema hata kama mtu ana ukimwi na Mungu bado ana kazi naye hapa duniani, hakika atamponya huo ukimwi na atampa mke au mme.
Faida na lengo la kupima ni hili, hata kama majibu yatatoka mmoja ameathirika isiwe mwanzo wa ninyi kuachana. Kama mna uhakika Mungu aliwaanganisha huu ndio wakati wa kurudi mbele za Mungu kwa maombi ya uponyaji na kujipanga zaidi juu ya hilo.
Jambo la saba – ni wakati wa kuongeza ufahamu wenu kuhusu nafasi yako kwenye ndoa.
Je umeshawahi kujiuliza ni kwa nini Mungu anakupa mke au mme? Yamkini zipo sababu nyingi lakini baadhi yake ni; Mungu anakupa mke kama msaidizi, mlinzi, na pia unapopata mke au mme unakuwa umejipatia kibali kwa Bwana na pia ni kwa sababu ya zinaa ndio maana unahitaji mwenzi. Hizi ni baadhi ya sababu zilizoko ndani ya Biblia. Hivyo basi tafuteni wanandoa mnaowaamini na zaidi waliokoka  muwaulize   kuhusu wajibu  wa kila mmoja kwa nafasi yake kwenye ndoa. Katika hili baadhi ya makanisa  huwa yana utaratibu wake wa nani atahusika na maelekezo ya aina hii kwa wachumba. Hivyo kama kanisa lako lina utaratibu huo, fuata huo utaratibu.
Katika ndoa kuna mambo mengi sana ambayo mtatakiwa kufanya, ni vema kufuata mwongozo na ushauri wa viongozi wenu au wachungaji wenu kuhusu nini mnatakiwa kufanya katika ndoa yenu. Angalizo hapa ni hili, uwe makini na vyanzo vya ushauri au mafunzo katika eneo hili ili lisije kuleta madhara baadae. Usitafute wala kufuata kila ushauri, bali sikiliza pia uongozi wa Mungu ndani yako.
Jambo la nane– Msifanye tendo la ndoa, maana jambo hili litaharibu mpango wa Mungu na kusudi lake kupitia ninyi.
Wakati wa uchumba, si wa kufanya mapenzi au kufanya michezo ya mapenzi. Tunarudia tena ili kuonyesha msisitizo kwamba chonde chonde jamani, uchumba sio ndoa, maana uchumba unaweza kuvunjika. Hairusiwi kabisa kwa wachumba kufanya mapenzi kwa maana ya tendo la ndoa kabla ya ndoa. Kitendo cha Mungu kukujulisha/kukupa huyo mwenzako kama mke/mume mtarajiwa haina maana mna haki ya kufanya mambo ya wanandoa. Mungu kukupa huyo mwenzako sasa ni taarifa kwamba  huyu ndugu ndiyo atakuwa mkeo au mmeo na anakupa taarifa sasa ili ujipange kufanya mambo ya msingi mnayotakiwa kuyafanya katika kipindi cha uchumba. Kipindi cha uchumba ndicho kipindi ambacho wachumba wengi sana wanavuruga kusudi la Mungu, na kuharibu maisha yao ya baadae na ndoa yao kwa ujumla.
Ndoa nyingi sasa hivi zina migogoro kwa sababu wakati wa uchumba walidiriki kufanya tendo la ndoa. Vijana wengi hawajajua kufanya tendo la ndoa kipindi cha uchumba lina madhara gani kwao na ndio maana wengine wanafanya. Biblia inasema katika Mithali 6:32 “Aziniye na mwanamke hana akili kabisa, afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake mwenyewe”. Hata kama ukifanya tendo la ndoa na mchumba wako ambaye mlibakiza siku moja kufunga harusi, bado umezini.
Ndani ya nafsi ya mtu kuna akili, hisia, nia na maamuzi. Biblia inaposema afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake ana maana hii, dhambi hii inapofanywa, ina haribu mfumo wa utiifu na uamnifu kwa Mungu wako, inapelekea kukosa usikivu wa rohoni kabisa, ina haribu mfumo wa kufikiri, kunia na kufanya maamuzi. Na kwa sababu hiyo si rahisi tena kusikia na kutii uongozi wa Roho Mtakatifu. Kwa watu ambao wamezoea kuwa na mahusiano mazuri  na Mungu watanielewa ninachosema hapa.
Zaidi kuna baadhi ya wachumba kweli hawafanyi tendo la ndoa bali wanafanya michezo ya mapenzi. Michezo ya mapenzi (Fore play) ni maalum kwa ajili ya wanandoa, na ni sehemu ya tendo la ndoa. Hivyo kufanya michezo ya mapenzi ni kufanya mapenzi kwa sababu ile ni sehemu ya mapenzi. Kuna vitu unavichochea,  unaamusha hamu ya mapenzi au unayachochea mapenzi. Biblia inasema katika Mhubiri 2:7 “Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, kwa paa na kwa ayala  wa porini, msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, hata yatakapoona vema yenyewe.”
Mungu pia anachukia michezo ya mapenzi soma Isaya 57:4-5 “Mnafanya dhihaka yenu juu ya nani, juu ya nani mmepanua vinywa vyenu, Na kutoa ndimi zenu? Je, ninyi si wana wa uasi, uzao wa uongo; ninyi mnaowasha tamaa zenu kati ya mialoni, chini ya kila mti wenye majani mabichi….. Wachumba wengi hawajui haya kwa sababu si makanisa yote yanayofundisha maswala ya mahusiano ya wachumba kimpana.
Mpaka hapa tunaamini umeshajua hasara za jambo hili  na utazijizuia kabisa kulifanya. Michezo ya mapenzi ni pamoja na kunyonyana ndimi, kushikana sehemu ambazo zinaamsha ashiki ya mapenzi kama sehemu za siri, matiti, kiuno nk, pamoja na kuangalia picha za ngono. Katika kipindi ambacho tumemtumikia Mungu kupitia vijana tumejifunza na kukutana na kesi mbalimbali za aina hii na kuona namna Shetani anavyovuruga mpango wa Mungu kwa vijana. Mwenye sikio na asikie neno ambalo Roho wa Bwana awaambia vijana ili kulida kusudi la ndoa.
Ni imani yetu kwamba mambo haya nane yameongeza ufahamu na hivyo kuwa maarifa ya kutosha kukusaidia kuenenda kwa mapenzi ya Mungu katika kipindi cha uchumba.

No comments: