IJUE BIBLIA | LISTENING GOD'S VOICE THROUGH GOSPEL SONGS


Breaking News

Wednesday, 14 September 2016

UCHUMBA WA KUFANIKIWA

UCHUMBA WA KUFANIKIWA

Kanuni 10 za Uendeshaji wa Uchumba

Picture
Kwanza

Wewe na mwenzako mnaweza kuwa na sifa nyingi kama wachumba. Huenda mkijitazama na watu wakiwaona, hakuna anayetilia mashaka kwamba mna wasifa na mmekomaa tayari kwa ndoa. Lakini kama dereva yeyote aliye na sifa anavyopaswa kuzingatia sheria za udereva, mnapaswa kuzingatia kanuni za uendeshaji uchumba. Zipo kanuni nyingi. Lakini kanuni hizi chache naziona zimebeba uzito usiopungua busara na maarifa ya kimbingu:

1. Mruhusuni Mungu awe Mjenzi mkuu wa uchumba wenu

Bwana asipoijenga nyumba Waijengao wafanya kazi bure. (Zab 127:1)

Wachumba wanaomkaribia Mungu huishia kukaribiana wao kwa wao. Mungu akiwa juu ya pembe tatu, umbali baina yao hupungua kila mmoja anapomkaribia Mungu. Tafuteni muda wa kusoma vitabu vya uvuvio na kuomba pamoja, nanyi mtauweka uhusiano wenu katika msingi imara.

2. Uwekeni uchumba wenu wazi mbele ya watu wanaowapenda

Bwana akamwambia Kaini, Yuko wapi Habili ndugu yako? Akasema, Sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu? (Mwa 4:9)

Tambua kuwa wanandugu wanaowapenda ninyi ni walinzi wa kuaminika wa njozi zenu za baadaye. Waruhusuni wazazi wenu, ndugu zenu na rafiki zenu waufahamu na kuukaribia uchumba wenu. Uchumba si siri. Msiwaweke mbali nanyi wanaowatakia mema maishani—hao ni walinzi wenu wa kuwaangalia, msiwafiche. Wanaweza kuwasaidia kuyaona msiyoyaona. Kumbukeni, nyani haoni kundule.

Picture
3. Jichanganeni na jamii katika shunguli za jamii

Hata alipokwisha kumnywesha akasema, Na ngamia zako nitawatekea, hata watakapokwisha kunywa. Akafanya haraka, akamwaga maji ya mtungi wake katika birika, akapiga mbio kisimani ateke, akawatekea ngamia zake wote.Basi yule mtu akamkazia macho…(Mwa 24:19-21)

Unapotumikia wengine unajianika ulivyo. Rebeka alipomsaidia mgeni asiyemfahamu hakujua anajitangaza kwa mshenga. Na mshenga alipopokea msaada wa Rebeka, hakuchelewa kumvika pete ya uchumba kwa niaba ya Isaka, mme mtarajiwa.

Wewe na mchumba mwenzako mnapojumuika na familia zenu, majirani wenu, au waumini wenzenu katika kazi mbalimbali mtapata fursa ya kufahamiana zaidi ninyi kwa ninyi. Utang’amua sura mpya ya mwenzako anapojichanganya na wengine katika mazingira ya kazi tofauti na mnapokuwa wawili tu.

Picture
4. Lindeni majina yenu yasiingie madoa

Heri kuchagua jina jema kuliko mali nyingi; Na neema kuliko fedha na dhahabu. (Mith 22:1)

Msijiachie kwenye majaribu ya mapenzi na kuruhusu majina yenu yapakwe madoa ya kashfa. Bora uwe muoga kuvunja miiko ya maadili kuliko jasiri kujiachia na kuchafua jina lako. Uchumba wenu ukiheshimiwa na watu, ndoa yenu itapanda thamani machoni penu na mbele ya jamii—hata hakuna kati yenu atakayeona rahisi kutilia mashaka kwamba Mungu habariki mipango yenu.

5. Msiwashane moto wa mapenzi msioweza kuuzima

Maji mengi hayawezi kuuzimisha upendo, Wala mito haiwezi kuuzamisha (Wimb 8:7) Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, Hata yatakapoona vema yenyewe (Wimb 2:7)

Japo si ajabu kwa wapendanao kuoneshana hisia kuwa wanapendana; lakini, hisia hizo zinapaswa zioneshwe kulingana na kiwango na mipaka ya uhusiano uliopo.  Kubalianeni miiko ya kuizingatia. Msiwe mabubu. Badala ya kuhisia kimyakimya,ongeeni wazi wazi. Kila mmoja ajue maeneo yasiyoingiliwa. Mnapochora pamoja mstari mwekundu usiopaswa kuvukwa kama wachumba, na kila mmoja akawajibika kuiheheshimu basi uhusiano wenu utazidi kupanda thamani machoni penu wenyewe.

Picture
6. Fungukeni mioyo na ongeeni kwa uwazi bila kufichana

Hata mpumbavu akinyamaza, huhesabiwa hekima; Akifumba midomo yake, huhesabiwa ufahamu. Mithali 17:28
Basi uvueni uongo, mkaseme kweli kila mtu na jirani yake; kwa maana tu viungo, kila mmoja kiungo cha wenzake. Waef 4:25


Kuwa huru na wazi kwa mwenzako kadri uhusiano wenu unavyosonga ili mzidi kufahamiana. Ukifungua moyo wako wazi mno na mapema mwanzoni mwa uhusiano wenu utamshtua mwenzako (hutuvui nguo kwa mgeni). Lakini pia ukiufunga moyo wako na kumzuia mwenzako asichungulie kurasa za maisha yako, mwenzako atashindwa kukukaribia (mficha uchi hazai). Funguka moyoni apate kukujua. Kadri unavyofunguka ndivyo naye atafunguka na pamoja mtazidi kufahamiana.

7. Malizeni tofauti zenu kistaarabu mara zinapojitokeza

Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka. Waef 4:26

Usikae na kinyongo moyoni. Uchungu ni sumu inayommaliza kwanza anayeitunza moyoni kabla haijamjeruhi yeyote aliye karibu. Mwageni yote machungu ya moyoni katika meza ya mazungumzo. Zungumzieni tofauti zenu kwa uwazi kama watu mnaoheshimiana.

Ongea uso kwa uso mkiangaliana na si nyuma ya mgongo wa mwenzako. Ongea wakati hisia kali zimepungua, na katika mazingira tulivu. Jifunzeni kugongea katika namna ambayo mwenzako atakuelewa.

Usipuuzie. Usidhani magugu ya uchungu moyoni yanajiozea unapopuuzia kuyazungumzia. Anika mambo yote mbele ya jua la ukweli kabla hujawa na hakika ya kuwa tofauti zenu zimesawazishwa.

8. Chagueni wanandoa waliowatangulia watakaolea uchumba

Pasipo mashauri taifa huanguka; Bali kwa wingi wa washauri huja wokovu. (Mith 11:14)

Hamna sababu ya kubahatisha pa kukanyaga na mwishowe muanguke kama wapo waliowatangulia wanaweza kuwaelekeza njia salama. Tafuteni wanandoa ambao wote mnavutiwa nao kama mfano wa kuigwa na kuwafanya kama walezi wa uchumba wenu. Wazazi wanaweza kufaa; lakini na wengine pia. Wawe walezi ambao mpo huru kwao kuwaeleza mashaka na hofu mlizo nazo. Wazazi wanaoweza kuwashauri maswala ya utawala wa fedha, uhusiano na wanandugu, uzazi wa mpango, tendo la ndoa na kadharika.

Haitoshi kusoma vitabu au kuhudhuria semina za uchumba. Jifunze pia kutoka kwa maisha halisia hai ya wanandoa wengine ili uongeze ujuzi wa ndoa.

Picture
9. Kila mmoja ajifunze kuongea lugha ya upendo ya mwenzake

Amri mpya nawapa, Mpendane (Yoh 13:34) Mchukuliane mizigo na kuitimiza hivyo sheria ya Kristo. (Gal 6:2)

Kila mmoja wenu ana lugha ya upendo aliyokuzwa nayo. Unaitumia kirahisi kuonesha unapenda na ikitumika unahisi kupendwa. Si rahisi wapenzi wawili wakutane wanaongea lugha moja ya mama. Gundua lugha yako kwa kujiuliza: Nimezoeaje kuonesha upendo kwa wengine? Mara nyingi ninanungunikia nini? Muda mwingi ninaomba nini? Ukimgeuzia mwenzako maswali hayo hayo utagundua lugha yake. Jambo la muhimu ni kupenda katika namna ambayo mwenzako atakuelewa unampenda

Nategemea kila mmoja wenu atakuwa anatumia mojawapo ya lugha hizi kuu za upendo kama zilivyofafanuliwa na Dr Gary Chapman. Nitazijadili kwa undani wakati mwingine. Lakini kwa sasa nizitaje, nazo ni: (a) lugha ya maneno ya kujali, (b) lugha ya kupeana zawadi, (c) lugha ya kusaidiana, (d ) lugha ya kutumia muda mwafaka pamoja na (e) lugha ya mguso wa upendo (miguso salama na inayokubalika). Unapojifunza kumpenda mwenzako zaidi ya ujuavyo wewe na kama ajuavyo yeye utakuwa unatekeleza vilivyo sheria ya Kristo.

10. Ingia katika uhusiano wa uchumba kama upo tayari kwa ndoa

Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu (Mhu 3:1)

Kusudi la uchumba chini ya mbingu ni kukuandaa wewe na mwenzako kwa ndoa. Kama unachumbia hata kwa kuzingatia kanuni tajwa hapo juu lakini hauko tayari kwa ndoa basi uhusiano wenu hauna maana. Ingia katika uchumba kama muda umewadia. Ingia kwenye uchumba na mtu unayedhani anaweza kuwa mwenzi wa maisha. Kuingia katika mahusiano na mtu yeyote kwa sababu amekuvutia kimwili lakini huoni anafaa katika maagano ya milele si salama. Usicheze na mkondo wa mapenzi unaopita kwa kasi. Utajitambua baada ya kunywa maji.

Picture9. Kila mmoja ajifunze kuongea lugha ya upendo ya mwenzake

Amri mpya nawapa, Mpendane (Yoh 13:34) Mchukuliane mizigo na kuitimiza hivyo sheria ya Kristo. (Gal 6:2)

Kila mmoja wenu ana lugha ya upendo aliyokuzwa nayo. Unaitumia kirahisi kuonesha unapenda na ikitumika unahisi kupendwa. Si rahisi wapenzi wawili wakutane wanaongea lugha moja ya mama. Gundua lugha yako kwa kujiuliza: Nimezoeaje kuonesha upendo kwa wengine? Mara nyingi ninanungunikia nini? Muda mwingi ninaomba nini? Ukimgeuzia mwenzako maswali hayo hayo utagundua lugha yake. Jambo la muhimu ni kupenda katika namna ambayo mwenzako atakuelewa unampenda

Nategemea kila mmoja wenu atakuwa anatumia mojawapo ya lugha hizi kuu za upendo kama zilivyofafanuliwa na Dr Gary Chapman. Nitazijadili kwa undani wakati mwingine. Lakini kwa sasa nizitaje, nazo ni: (a) lugha ya maneno ya kujali, (b) lugha ya kupeana zawadi, (c) lugha ya kusaidiana, (d ) lugha ya kutumia muda mwafaka pamoja na (e) lugha ya mguso wa upendo (miguso salama na inayokubalika). Unapojifunza kumpenda mwenzako zaidi ya ujuavyo wewe na kama ajuavyo yeye utakuwa unatekeleza vilivyo sheria ya Kristo.

10. Ingia katika uhusiano wa uchumba kama upo tayari kwa ndoa

Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu (Mhu 3:1)

Kusudi la uchumba chini ya mbingu ni kukuandaa wewe na mwenzako kwa ndoa. Kama unachumbia kwa kuzingatia kanuni zilizotajwa hapo juu lakini hauko tayari kwa ndoa basi uhusiano wenu hauna dira wala maana. Ingia katika uchumba kama uko tayari kwa ndoa. Usiingie kwenye uchumba na mtu unayedhani hawezi kuwa mwenzi wa maisha.

Kuingia katika mahusiano na mtu yeyote kwa sababu amekuvutia kimwili lakini huoni anafaa katika maagano ya milele ni utapeli na unajidanganya mwenyewe. Ukinogewe je? Usicheze na mkondo unaopita kwa kasi. Ukijaribu, baada ya kunywa maji ndipo utakapozinduka. Na utakuwa na bahati kama utabakia hai kuzinduka.

No comments: