IJUE BIBLIA | KNOW THE BIBLE
KUADABISHWA NA MUNGU
Bwana Yesu asifiwe…
Kwa ufupi.
“kuadabishwa” ni aina ya nidhamu inayotolewa hasa na mzazi kwa mtoto wake. Kitendo hiki cha kumnyoosha mtoto aliyekosa ili aweze kumwelekea vyema babaye,au afuate utaratibu stahiki kwa upendo,huitwa “kuadabishwa “,hata hivyo; Biblia inalitumia neno hili kuonesha ya kwamba Mungu naye hutuadabisha kama njia ya kuturejeza kwenye mstari sahihi. Wakati mwingine biblia hutumia neno “marudia” kuwakilisha namna ya kuadabishwa.
Ukweli ni kwamba,yeyote unayempenda ni lazima utamrudi / yaani umfundishe nidhamu kwa bakola ya kumnyoosha kwa upendo kabisa . Na ikiwa kama hutoi nidhamu kwa mtu ambaye umpendaye,basi haumpendi,kwa maana usipomfundisha nidhamu basi ujue atakuharibikia mkononi mwako huku ukimwona. Hata Mungu anatupenda sana,kiasi kwamba kwa pendo lake hataki tupotee au kuharibika kwa sababu hiyo inamlazimu atuchape kwa bakola za kibinadamu.
“ Maana yeye ambaye Bwana ampenda, humrudi,Naye humpiga kila mwana amkubaliye.Ni kwa ajili ya kurudiwa mwastahimili; Mungu awatendea kama wana; maana ni mwana yupi asiyerudiwa na babaye?“ Waebrania 12:6-7
Hakuna mwana asiyeadabiswa na babaye. Ebu fikiria kipindi cha utoto,ambapo baba yako alikuwa akikuchapa ili uende shule,na unapokosea kosea darasani baba alikuwa hakuachi bali anakuchapa na kukufuatilia sana huko shuleni wakati mwingine hutembea na bakola kucheki kama kweli umekwenda tuisheni au la,akigundua umetega hukwenda,basi hapo atakuchapa bakola mtindo mmoja. Lakini bakola hizo anazokuchapa atahakikisha hakupigi usoni,wala hakupigi ngumi ya uso,isipokuwa bakola za makalio. Kwa sababu anakupenda.
Lakini tazama sasa umekuwa mtu mzima na kwa bakola za mzee zimekufanya leo unaitwa msomi,zimekupeleka mahali fulani. Sasa katika mazingira kama hayo,fikiria kama mzee angekuchekea chekea pale ulipokataa masomo! Je leo hii ungelikuwa wapi? Ungeliitwa msomi? Lah hasha,ulihitaji bakola za baba yako zikufikishe hapo ulipo.
Ikiwa ndivyo,Mungu je? Maana Yeye hutupenda zaidi ya baba wa damu,hivyo ni lazima aturudi zaidi ili tufike kwenye eneo fulani zuri. Na ukumbuke kama Mungu anakuleta kwenye mstari sahihi lazima atakuchapa tu ila ni kwa fimbo ya kibinadamu kabisa, kwa mfano; unaweza ukajikuta unaumwa kama sehemu ya bakola ya Mungu ya kukurejeza ili ukae vizuri,ili usimtukane Mungu tena kwa maneno au matendo yako. Au unaweza unajikuta mambo yamefunga kila kona kama sehemu ya bakola ya Mungu ili urejee. N.K
Hata hivyo,tambua kwamba ; Kuadabishwa sio kuadhibiwa kwa maana neno “adhabu” lipo tofauti na neno “nidhamu “,kwa maana kupata adhabu huleta maumivu,mateso na kusababisha kulipa kisasi,isipokuwa kupata nidhamu kuna lengo la kumfundisha mkosaji kwa upendo,kwa lengo zuri kabisa tena pasipo kusababisha madhara. Mfano; mtoto anapokukosa na ukaamua kumsema au ukamchapa kwenye makalio kwa fimbo laini kwa lengo la kumfanya ashike adabu,huitwa unamfundisha nidhamu / unamwadabisha.
Lakini pale anapodiliki kumpiga mtoto hata kumuumiza,iwe kwa ngumi au makofi au kifaa chochote hata kusababisha uchungu na hasira ndani ya mtoto,hapo una mwadhibu/ hiyo huitwa “adhabu “. ( ebu fikiria unampiga mtoto kwa kuni au mwiko,au unamrushia jembe,huku ni kuleta madhara na ndio huitwa adhabu). Biblia haisemi kuwaadhibu watoto pale wanapokosea bali kuwapa nidhamu.
“Usimnyime mtoto wako mapigo;Maana ukimpiga kwa fimbo hatakufa.” Mithali 23:13
Nasi tunapokuwa mbele za Bwana,tunastahili kuadabishwa ikiwa kama tunamkosea Yeye mwenye huruma. Wakati mwingine tunafikiria ni shetani,lakini si wakati wote;kwa maana njia zetu pia zinamhuzunisha Mungu, naye hutupatia nidhamu stahiki. Ebu chukulia mfano wa mtu ambaye anaijua kweli lakini hupenda kufanya dhambi tena anafanya hali akijua ni dhambi na kisha hufurahia dhambi, mtu huyu hawezi kuachwa vivi hivi,ni lazima apigwe kama nidhamu,ili asiizoee dhambi.
Kuna kipindi Bwana alisema na mfalme Daudi kwa habari ya uzao wake hasa Suleimani. Maana Daudi alitaka kumjengea nyumba Mungu, sasa Bwana akasema naye kwa kinywa cha Nabii Nathani. Akamwambia wazi wazi kwamba yeye Daudi hatajenga hekalu isipokuwa mwanae Suleimani ndiye atakayejenga,lakini akitenda uovu,atachapwa kama mkosaji;
“ Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu; akitenda maovu nitamwadhibu kwa fimbo ya binadamu na kwa mapigo ya wanadamu;” 2 Samweli 7:14
Bwana anapokuchapa haina maana hakupendi,bali ina maana anakupenda ndio maana unapewa bakola zako. Bakola hazifuti wala kuondoa pendo lake kwake,anakupenda tu,ingawa wewe hujali.
Kitu gani cha kufanya usipewe nidhamu (usiadabishwe)
- Kujitahidi kutii.
Hakuna njia nyingine ya kukwepa kurudiwa isipokuwa ni katika kutii sauti yake na maelekezo yake yote. Na Mungu amewaweka wachungaji kusimama badala yake,wachungaji wasiposikilizwa maana yake sauti ya Mungu haikusikilizwa. Sasa ili usikie vyema utahitaji bakola zake kama sehemu ya mtoto mbele zake. Hivyo kabla ya kumkemea shetani,ni vyema ukatafakari njia zako maana wakati mwingine ni bakola tu zinakufanya hivyo na wala sio shetani. Ndio maana kabla ya kuanza maombi ya kubomoa na kuvunja kazi za ibilisi,anza na toba mbele za Bwana. Wengi leo wamechapwa kwa fimbo na Mungu na bahati mbaya wakidhani aliyewachapa ni shetani!
Lakini ukitafakari maisha yao kwa kina utagundua katika hayo yote kuna mkono wa Mungu pia kama sehemu ya kuwanyoosha ili warudi kwa Bwana kwa kuwa wamekuwa ni watu wa makosa ya mara kwa mara tena kwa makusudi kabisa. Tafakari sasa kwenye maisha yako,kisha ingia kwenye toba.
No comments:
Post a Comment