IJUE BIBLIA | KNOW THE BIBLE
NJIA YA HAKI
Kwa ufupi.
Bila shaka kama ikiwapo njia ya haki basi ni dhahili njia ya uovu na yenyewe itakuwepo tu. Na kama kuna njia uovu / ubaya basi kabla ya kujua njia ya haki,ni vyema ukaijua njia ya uovu. Neno “ njia” kama linavyotumika kwenye biblia halina maana ya njia kama barabara tulizonazo ambazo tunatembelea. Kumbuka; Biblia inajaribu kusema nasi katika lugha ya picha,lugha raisi ya kibinadamu ili kusudi upate kuelewa vizuri. Hivyo,neno “ njia” ni “mfumo binafsi au taratibu binafsi“. Inawezekana ukawa ni mfumo binafsi wa maisha ya mtu,au taratibu zinazofuatwa na mtu binafsi. N.K
“Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu,Lakini mwisho wake ni njia za mauti.“Mithali 14:12
Andiko hili ni sawa na kusema “upo taratibu fulani / mfumo binafsi wa maisha ya mtu unaonekana sawa machoni pake,Lakini mwisho wa mfumo huo ni uharibifu / maangamizo/ mauti“
Ikiwapo taratibu fulani ya maisha yako uliyochagua kuishi,ujue hiyo ni njia. Lakini je ni taratibu gani uliyonayo? Bila shaka taratibu za maisha binafsi ya mwanadamu ni mbaya tu siku sote,kwa sababu mawazo yetu ni mabaya kama Mungu hajausika hapo. Katika mfumo binafsi wa maisha ya mtu mwovu siku zote hujiona yeye yupo sahihi sana kuliko anavyoonekana. Na huo ndio ukweli wenyewe!! Hujawahi kuona mtu ambaye mtenda uovu akijitetea kwamba yeye hana makosa,ila makosa anasingiziwa!! Lakini ujue mtu huyu akishupaza shingo wakati wa kuonywa ujue atavunjika na kukosa dawa ( Mithali 29:1)
“ Ingieni kwa kupitia mlango ulio mwembamba; maana mlango ni mpana, na njia ni pana iendayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa mlango huo.Bali mlango ni mwembamba, na njia imesonga iendayo uzimani, nao waionao ni wachache.” Mathayo 7:13-14
Andiko hilo,nataka nikutazamishe neno “njia” kama lilivyotumika. Neno njia ,bado linatupa maana ile ile kwamba ni mfumo wa maisha. Kwamba mfumo wa maisha ya watu unaowaingiza watu wengi motoni ni mpana ( yaani watu wengi wapo kwenye mfumo au taratibu hizo,za maisha ya kila siku)
Lakini pia “njia” / taratibu ni ndogo,zinazowapeleka watu mbinguni ( si wengi wanaoishi kwenye taratibu sahihi za kiungu,na wengi hukosa taratibu hizo.)Watu wengi wamejikuta wakiishi maisha kama fulani aishivyo. Au watu uishi kama dunia itakavyo. Na huku ndiko kunakoleta matokeo ya mauti mwishoni.
Macho yanatabia ya kudanganya siku zote na ndio maana unaweza ukaona njia unayopita ni sawa lakini mwisho wake ni uharibifu mkubwa. Katika hili,mtu yeyote akiishi kufuata mwili kwa kile akionacho,atapotea tu. Biblia inazidi kutuambia kwamba “amebarikiwa mtu yule asiyekwenda kwenye njia ya wakosaji ” ( Zab.1:1). Hii ina maana kwamba, ikiwa utafanikiwa kuwakimbia watendao maovu kwa namna yoyote ile,kwa mfano kuwakimbia watu wenye mizaha,makundi ya watu wasengenyaji n.k,basi u heri wewe,yaani umebarikiwa.
Lakini ebu jiulize katika hili kwamba ni mara ngapi umekuwa ukishiriki vikao vya watu waovu? Ni mara ngapi unashiriki kupiga gumzo na waovu? Ujue jambo moja ya kwamba ikiwa kama utakuwa pamoja na watu wa namna hii mara kwa mara,basi ni lazima utashuka kiwango chako cha kiroho,na utamchukiza Bwana. Ninajifunza kitu ninapoyatafakari maisha ya Daudi mtu aliyeupendeza moyo wa Mungu. Lakini mtu huyo huyo,kuna kipindi alijisahau na kujikuta akiiacha njia ya Bwana kwa maana alilala na mke wa jemedari wake kisha akamuua huyo jemedari. Biblia inasema Daudi alitubu,kisha baada ya toba Daudi alitamani kutoka na kuwafundisha wakosaji waliokuwa wakitembea kwenye njia za mauti. ( Zab.51:13).
Daudi alitamani wakosaji wasije kuanguka zaidi kama alivyoanguka. Huu ndio moyo unaopaswa kuumbika ndani yako;kwamba unapowaangalia wakosaji utamani uwafundishe njia ya haki,ili waiche njia zao mbaya! Lakini,jihoji kwamba ndivyo ufanyavyo? Au ndivyo tunavyofanya leo? Kwa maana leo kile kinachofanyika ni kwamba kila mmoja ni mbinafsi hivyo tumejikuta wengi tunaomba Mungu atusamehe sisi tu na tukimaliza hatuna haja ya kuwaendea wakosaji ili na wao wasamehewe pia.
- Njia ya haki ni ipi hiyo?
Neno “haki” kibiblia ni kuwa na uhusiano mwema na Mungu. Biblia inatusaidia kutupa maana ya “njia ya haki ” kwa kumweleza Yesu kuwa “Yeye mwenyewe ni njia” ( Yoh.14:6). Hii ikiwa na maana kwamba Yesu haoneshi njia,bali Yesu mwenyewe ndiye njia. Maana kuna utofauti ya mtu kuonesha njia na mtu binafsi kuwa njia.
Ikiwa Yesu mwenyewe ndiye njia hii ina maana mtu anayetaka kuja kwa Baba ni lazima tembee kwenye njia ambaye ndiye Yesu. Hivyo njia ya haki, ni utaratibu uliowekwa sahihi wa kutembea na Mungu. Ikiwa mtu mmoja akiita neno moja hili “wokovu” atakuwa hajakosea.Mungu ameweka utaratibu sahihi wa maisha kwa msaada wa Roho mtakatifu.
Kumbuka hili,mtu yeyote akiwa mbali na uso wa Mungu basi yupo mbali na njia ya haki. Na kwa sababu hiyo mtu huyo yupo huru mbali na haki. ( Warumi 6:20-21). Hii ina maana kwamba mtu ambaye yupo mbali na njia ya haki u mtumwa wa dhamb,na akiwa mtumwa wa dhambi basi ni sawa na kusema yupo na uhuru wa kutenda dhambi. Mfano; hujawahi kumwona mtu ambaye anaweza kujinyima kitu fulani ili makusudi atende dhambi? Au mtu ambaye yupo radhi apoteze gharama fulani kwa ajili ya kuipata dhambi fulani?? Ndio wapo,sasa watu wa namna hii ni watumwa wa dhambi nao wana uhuru mbali na haki.Ikiwa kama unahitaji kumwishia Kristo,huna budi kutembea kwenye njia ya haki kwa kuokoka kwanza kama sehemu muhimu sana.
Ifike wakati ujikague njia zako,upoje kwenye njia zako? Je upo kwenye njia ya Bwana? Je mfumo wa maisha yako unayoishi unampendeza Mungu? Vipi kama akija leo Kristo,utakwenda mbinguni au motoni,? Ukijihoji vizuri utagundua kwamba kuna mahali unahitaji kutengeneza na Mungu tena mapema kwa sababu usipofanya hivyo,lipo anguko mbele ya njia yako. Maneno haya ni muhimu kuyafanyia kazi.
No comments:
Post a Comment